Kwa mujibu wa Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Sheikh Zuhair Ja‘id, Mratibu Mkuu wa “Jabhatu al-‘Amal al-Islami nchini Lebanon”, alishiriki katika Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Kidini uliofanyika katika mji wa Saint Petersburg nchini Urusi, kwa kaulimbiu: “Maadili ya Kiroho na Jadi: Changamoto za Kisasa na Mikakati ya Kuyaimarisha”, ukishirikisha wasomi mashuhuri miongoni mwa maulama, wanazuoni wa dini, wanafikra na wawakilishi wa dini na tamaduni mbalimbali.
Sheikh Ja‘id, katika hotuba yake katika kikao cha jumla cha mkutano huo, alisisitiza kwamba: Migogoro ambayo dunia inashuhudia leo haiishii tu katika nyanja za kisiasa, kiuchumi na kiusalama, bali kabla ya yote inahusiana na mgogoro wa mwanadamu, maadili na maana. Maendeleo ya kisayansi na kiteknolojia pekee hayatoshi kuijenga dunia salama, isipokuwa yaambatane na kuweka misingi ya haki, huruma, heshima kwa utu wa mwanadamu na utukufu wa uhai.
Sheikh Ja‘id alisisitiza: Dini haipaswi kubadilishwa kuwa chombo cha migogoro baina ya wanadamu, bali inapaswa kubaki kuwa ujumbe wa uongofu, huruma, mizani ya haki na mlinzi wa utu wa mwanadamu. Alitoa wito wa kuimarisha mazungumzo baina ya wafuasi wa dini na madhehebu mbalimbali, sambamba na kuhifadhi misingi na itikadi.
Alisema: Mazungumzo hayamaanishi kukubaliana katika kila jambo, bali yanamaanisha kuwa na uwezo wa kutofautiana bila kuzigeuza pande zinazotofautiana kuwa maadui wao kwa wao. Kuwa wazi na kufanya mazungumzo hakupingani na kushikamana na itikadi na misingi.
Sheikh Ja‘id, katika hotuba yake, alizungumzia hali ya Lebanon na Palestina na kusisitiza kwamba: Taifa la Lebanon linastahili kuishi kwa usalama na heshima katika ardhi yake, mashambulizi dhidi yake yakomeshwe, na mamlaka yake pamoja na maisha ya watoto wake yalindwe. Aidha, alirejelea yale ambayo Lebanon imeyavumilia na ambayo bado inaendelea kuyavumilia kutokana na vita, mashambulizi na uvamizi, pamoja na gharama kubwa ambazo raia wamezilipa.
Alisisitiza: Palestina si suala la Waislamu pekee, bali ni suala la kibinadamu linalohusiana na haki, ukweli na utu wa mwanadamu. Alilaani yale ambayo taifa la Palestina linakabiliwa nayo, ikiwa ni pamoja na mauaji, kuhamishwa kwa nguvu, uharibifu na dhuluma, pamoja na kuvamiwa maeneo matakatifu ya Kiislamu na Kikristo, hususan Msikiti wa Al-Aqsa, Kanisa la Kiyama na Kanisa la Kuzaliwa, pamoja na misikiti, makanisa na maeneo mengine ya kidini.
Katika suala hili, Sheikh Ja‘id alisisitiza ulazima wa kuweka tofauti ya wazi baina ya Uyahudi kama dini ya mbinguni ambayo Waislamu wanaipa heshima na kuitambua, na Uzayuni kama mradi wa kisiasa; huku wakati huo huo akipinga aina yoyote ya kumtesa mwanadamu kwa sababu ya dini yake au utambulisho wake.
Sheikh Ja‘id, alipokuwa akizungumzia migogoro ya kimataifa, aligusia mzozo kati ya Urusi na Ukraine, akiamini kwamba ubabe wa kimataifa, uingiliaji wa mambo ya ndani kutoka nje, siasa za kulazimisha hali iliyokwishawekwa kuwa ukweli, pamoja na kujichukulia mamlaka ya kipekee katika maamuzi ya kimataifa, vimechangia katika kuongeza ugumu wa migogoro na kurefusha muda wake.
Alitoa wito wa kupitishwa kwa mtazamo wa mazungumzo na suluhisho za kisiasa, akakataa kugeuzwa damu na usalama wa mataifa kuwa nishati ya migogoro na maslahi ya kisiasa-kijiografia, na akasisitiza ulazima wa kuitanguliza mantiki ya amani na mazungumzo mbele ya mantiki ya vita na kuongezeka kwa mvutano.
Sheikh Ja‘id alisifu uzoefu wa Urusi katika kuheshimu utofauti wa kidini na kitamaduni, na kusema: Ushirikiano na Urusi pamoja na nchi zinazoheshimu maadili ya kidini na kimaadili na zinazokataa ubabe wa upande mmoja, unaweza kusaidia katika kuijenga dunia yenye nguzo nyingi za nguvu, yenye uwiano zaidi, haki zaidi na usalama zaidi kwa mataifa.
Mratibu Mkuu wa Jabhatu al-‘Amal al-Islami alitoa wito wa kuhuishwa kile alichokiita “diplomasia ya kidini”, ili nafasi ya taasisi za kidini na maulama isiishie katika kutoa taarifa na kuandaa mikutano, bali uwepo wao ugeuke kuwa hatua ya kweli ya kuleta amani, kuwalinda raia, kutetea maeneo matakatifu, kuyaleta karibu mataifa, na kukabiliana na chuki, ubaguzi wa rangi, misimamo mikali, ugaidi na Unazi mpya.
Pia alisisitiza ulazima wa kuanzisha ushirikiano wa kweli baina ya serikali, vyuo vikuu, taasisi za kidini na jamii, kwa lengo la kulea vizazi vinavyoijua dini yao, vinavyoheshimu sheria, vinavyomheshimu mtu mwenye mtazamo tofauti na wao na vinavyokataa vurugu. Aliongeza: Mwanadamu anayejiamini katika itikadi yake hana haja ya kuwachukia wengine.
Sheikh Ja‘id alisisitiza: Umoja wa Kiislamu ambao Jabhatu al-‘Amal al-Islami inautafuta ni umoja unaojengwa juu ya nguvu ya imani, uwazi na mazungumzo, si umoja unaojengwa kwa misingi ya kuwaondoa wengine.
Alisema: Kinachohitajika ni “uthabiti katika itikadi, uwazi katika mazungumzo, uwazi katika msimamo, huruma katika kushughulika na wengine, nguvu katika kukabiliana na dhuluma, na haki hata kwa upande wa pili.”
Mwisho wa hotuba yake, Sheikh Ja‘id alitoa wito wa kuufanya mji wa Saint Petersburg kuwa daraja la mawasiliano baina ya Mashariki na Magharibi, na baina ya dini na mataifa, akisisitiza: Dunia haihitaji kuta zaidi, bali inahitaji madaraja zaidi.
Alisisitiza: Ushindi mkubwa zaidi ambao dini zinaweza kuutolea ubinadamu ni pale ambapo mwanadamu ataishinda chuki, haki ishinde dhuluma, huruma ishinde ukatili na amani ishinde vita.
Makubaliano ya Ushirikiano kati ya Jabhatu al-‘Amal al-Islami na Utawala wa Kidini wa Waislamu wa Saint Petersburg
Pembeni mwa mkutano huo, na katika mfumo wa kuimarisha uhusiano wa Kiislamu na mawasiliano baina ya taasisi za kidini, Sheikh Ja‘id na Mufti wa Saint Petersburg, Sheikh Ravil Benchif, walitia saini makubaliano ya ushirikiano baina ya “Jabhatu al-‘Amal al-Islami nchini Lebanon” na “Utawala wa Kidini wa Waislamu wa Saint Petersburg.” Makubaliano hayo yanalenga kuimarisha ushirikiano, mawasiliano na kubadilishana uzoefu baina ya pande hizo mbili, kupanua nyanja za kazi za pamoja katika masuala ya kidini, kiakili na kiutamaduni, kuimarisha mazungumzo baina ya dini na madhehebu, na kuweka misingi ya maadili ya wastani, kuvumiliana na kuishi pamoja; kwa namna ambayo itahudumia umoja wa Waislamu na kuimarisha uwepo wa maadili ya kiroho na kimaadili katika kukabiliana na changamoto za jamii za kisasa.
Pande hizo mbili zilikokoteza kwamba kutiwa saini makubaliano haya ni hatua mpya katika njia ya kuimarisha madaraja ya mawasiliano na ushirikiano baina ya Lebanon na Urusi, na baina ya taasisi za Kiislamu za nchi hizo mbili, pia zilieleza kwamba jambo hili litafungua upeo mpana zaidi kwa ajili ya miradi na mipango ya pamoja katika hatua ijayo.
Maoni yako